Ball Dancer JR…Himid Mao Mkami

28 Nov

ImageHimid  Mao ni mtoto wa nyota wa soka wa zamani, Mao Mkami ‘Ball Dancer’ aliyewahi kuwa mchezaji wa Pamba ya Mwanza ,Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro na Moro United ya Morogoro.

Wadau wa soka wanakumbuka ‘Ball Dancer’, ambaye alipewa jina hilo na mtangazaji maarufu wa zamani wa Redio Tanzania, Charles Hillary.

Himid anafuata nyayo za baba yake kutokana na umahiri wake katika sehemu ya kiungo lakini kikubwa zaidi ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja.

Unaweza kumfananisha na nyota wa zamani kama Mtwa Kihwelo, Roster Ndunguru, Kenneth Mkapa, John Kabisama na wengine wengi.

Himid, ambaye ni maji ya kunde, mrefu ana mwili wa wastani, ni hodari uwanjani kutokana na kuhimili mikikimikiki ya mastaa wa Ligi Kuu Bara.

Jina lake lilikuwa ni miongoni mwa wanasoka wanaotarajiwa kufanya vizuri kwenye ulimwengu wa soka kwani alikuwa tegemeo kwenye timu za taifa za vijana wa chini ya miaka 17, 20 na 23.

Pia kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo alitambua uwezo wake na kumjumuisha katika kikosi chake kwa nyakati fulani.

Hata hivyo, msimu uliopita jina lake lilififia na wadau wa soka walikuwa wakihoji kupotea kwake lakini msimu huu amefanya kweli na kuibuka kivingine na kunasa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mserbia Boris Bunjak.

Kutokana na uwezo huo, Mwanaspoti ilifanya naye mahojiano na Himid alieleza historia yake, sababu ya kushuka na anavyojipanga kuhakikisha anafikia malengo aliyokusudia.

Kupotea na kuibuka kwake
Himid anasema masomo ndiyo yaliyokuwa sababu kubwa ya kumfanya apotee katika ulimwengu za soka.

“Najua sikuwa vizuri kipindi kilichopita lakini sasa nimerudi kwa kasi mpya ya kucheza mpira.

“Nilipotea kidogo kutokana na majukumu ya masomo niliyokuwa nayo. Mwaka jana nilifanya mtihani wa kidato cha nne, kwa hiyo maandalizi yake yaliathiri kiwango changu cha soka.

“Nimemaliza masomo, niko huru, wajibu wangu ni mmoja tu wa kucheza mpira.

“Nitajituma kwa nguvu zangu kwa kufuata maelekezo ya mwalimu na kwa ushirikiano mzuri wa wachezaji wenzangu naamini nitafanikiwa,” anasema Himid, aliyekuwa Shule ya Sekondari ya Tabata, Dar es Salaam.

Alivyochanganya masomo na soka
Kipaji cha Himid kilionekana tangu akiwa mdogo na kwa sababu hiyo ilibidi achanganye masomo na soka kwa wakati mmoja.

“Ilinibidi kufanya hivyo kwa sababu vyote ni muhimu kwangu. Masomo na soka ni muhimu kwa kuendeleza maisha yangu.

“Hata hivyo, sikuwa na tatizo kwa sababu vyote nilimudu licha ya kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja ni tatizo.”

Anasema kwa ugumu uliojitokeza ilibidi aelekeze nguvu zote katika masomo kwa lengo la kufaulu vizuri hali iliyosababisha kiwango chake uwanjani kishuke.

“Ugumu niliupata wakati najiandaa na mtihani kidato cha nne kwa sababu nilitaka kufaulu vizuri, ikanibidi kutumia muda wangu mwingi kwenye masomo na kusitisha mambo ya soka.”

Anasema wakati anasoma Tabata, alipata wadhifa wa kuwa waziri wa michezo wa shule hiyo na wanafunzi wenzake walikuwa wakimchukulia kawaida licha ya kuwa yeye tayari alishaanza kupata kipato cha kuendesha maisha yake kupitia mshahara wa kucheza soka.

“Sikujiona wa tofauti na wenzangu ndivyo walivyonichukulia tuliishi sawa kwa sababu mwenyewe nilijitambua kuwa ni mwanafunzi na nilitakiwa kufanya nini kwa wakati huo.

“Nilikuwa na bahati kwa sababu ya kwanza ya kusomeshwa na klabu yangu ya Azam.

“Hali hiyo ilisaidia kuwapunguzia gharama wazazi wangu lakini pia kama ningeamua kuachana basi ingebidi nijikite katika soka.”

Ameenda mbali na kuwausia vijana wengine ambao wana vipaji na kuwataka wasiache masomo kwa sababu elimu ni muhimu.

“Unajua kila kitu kina wakati wake na umuhimu wake lakini kitu chochote ukifanya ukiwa na elimu ya darasani lazima utafanikiwa kwa sababu utakuwa unajua unachokifanya.”

Ndoto yake
“Malengo yangu ni kufika mbali zaidi kupitia soka kama walivyofanikiwa wengine na naamini nitafanikiwa.

“Lakini ukiacha soka katika maisha yangu ya baadaye nataka kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa wa kimataifa.

“Kwa sababu hayo ndiyo malengo yangu mpango wangu hapo baadaye nitajiendeleza katika vyuo vya biashara ili kuinogesha kazi yangu iwe nzuri,” anasema Himid, ambaye mama yake, Asia na baba yake ndio waliokuwa mstari wa mbele kumsisitizia kuhusu elimu.

Alivyoibuka
Kuibuka na kukua kwa soka la Himid kwanza ni kutokana na urithi kutoka kwa baba yake, Mao Mkami ‘Ball Dancer’.

“Pamoja na kipaji cha mzee (Mao Mkami) wapo walimu waliofanikisha sehemu kubwa ya kipaji changu kwanza ni Mwalimu Berlin, alinifundisha kwenye kituo cha kukuzia vipaji cha Moro Youth,” anasema Himid na kituo hicho ndicho kimewaibua, Shomari Kapombe na Edward Christopher wote wa Simba.

Anasema alipokuwa akisoma Shule ya Msingi ya Dk. Omary Ali Juma, alijiunga na kituo cha kukuzia vipaji cha Elite Temeke ambacho kinamilikiwa na Mkuu wa Ufundi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni.

“Nilijiendeleza na Elite na 2007 nilichaguliwa kuunda timu ya Mkoa wa Temeke kwa ajili ya michuano ya Copa Coca Cola.

“Nikiwa na Temeke nilifanya vizuri nikachaguliwa kuunda timu ya kombaini ya Copa Coca Cola chini ya miaka 17 tukaenda kushiriki michuano ya dunia nchini Brazil.
“Wakati huo huo nikachaguliwa kwenye timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 na kushiriki michuano mbalimbali nikiwa na kocha Marcus Tinoco.

“Serengeti Boys ndiyo iliyonifungulia njia kwani nilivyokuwa najibidiisha uwanjani ndivyo nilivyopanda nikachaguliwa timu ya vijana chini ya miaka 20 na 23 hadi ya wakubwa ilipokuwa chini ya kocha Mbrazili Marcio Maximo.”

Hata hivyo, katika kipindi chote akiwa na timu za Taifa alikuwa tayari amejiunga na klabu ya Azam FC mwaka 2007 na aliitwa akitokea huko ambako alianza kulelewa katika kituo cha yosso cha klabu hiyo na baadaye akapandishwa ya wakubwa.

Himid anawazungumzia pia makocha wake, Tinoco na Maximo kuwa ni watu ambao wametoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango chake.

“Kwanza, Maximo ambaye kwangu namchukulia ni zaidi ya mwalimu na kwa upande mwingine naweza kusema ni mzazi kutokana na jinsi alivyokuwa anatulea.

“Alikuwa akitufundisha mambo mengi ya uwanjani lakini pia malezi nje ya uwanja,” anasema.

Himid ameenda mbali na kueleza mechi ambayo hatakuja kuisahau maishani mwake kuwa ni ya 2008 mwaka walipocheza na Kagera Sugar. “Hiyo ilikuwa mechi yangu ya kwanza kucheza Ligi Kuu lakini pia timu ilikuwa inahitaji pointi moja tusishuke daraja.”

Historia
Himid ni wa kwanza kuzaliwa katika familia yenye watoto watano. Ndugu zake wengine ni Femina, Rozmana, Faisal na Rahim.

Elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Msingi Kiwandani, Turiani, Morogoro darasa la kwanza na la pili na kuhamia Karume ya Dar es Salaam na alisoma hadi darasa la sita. Alihama tena na kumalizia elimu ya msingi

Shule ya Msingi ya Dk. Omary Ali Juma iliyopo Magomeni, Dar es Salaam kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Tabata ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 2011.

HIMID MAO MKAMI
Kuzaliwa: Novemba 5, 1992
Mahali: Dar es Salaam, Tanzania
Klabu: Elite Academy 2005-2007,
Azam FC 2007-
Taifa: Tanzania

Leave a comment